Wednesday, September 7, 2011

LINDA NDOA YAKO MWANAMKE, ISIJE KUPONYOKA BURE!

Familia mseto kama hizi kupinduana hutokea sanaUnapoishi nyumbani na ndugu yako, jamaa yako au hata mtumishi wa kike, ni vizuri ukajitahidi kulinda ndoa yako. Kumbuka kwamba, wanaume hawajali hisia, hujali zaidi mwili. Kama ukimwachia ndugu yako, jamaa au rafiki yako kumzoea sana mumeo, jua tu kwamba, inawezekana unajitengenezea maumivu makubwa sana hapo baadae.


Tafiti zinathibitisha sana kwamba, mwanaume anapohisi kuwa mwanamke fulani anamwonesha kwamba, yeye ni mwanaume kweli kweli, anapoonesha kwamba, anatambua uwepo wake na mchango wake katika familia, mwanaume huanza kumpenda, bila kujali sura au hadhi.Kama ndugu yako ni mjuaji wa mambo haya, anaweza kumwonesha mumeo kwamba, anaamini kuwa ni mwanaume kwelikweli. Hii hufanyika kwa kumsifu, kutopingana naye, kumpongeza mara kwa mara na kumwonesha kwamba anaamini katika yeye.Hata wale watumishi wa ndani, wanaochukuliwa na wanaume za watu hawafanyi hivyo kwa sababu, ati hao watumishi ni wazuri sana wa sura au wanajua sana mapenzi, hapana.Wanaume huwachukua kwa sababu, wake au wapenzi wa wanaume hao wameshindwa wajibu wao, wameshindwa kujua kwamba wanaume hutazama uhusiano kwa jicho tofauti.Lakini, iwe ndugu au jamaa zenu na hata watumishi majumbani mwenu, bado na wao ni binadamu, wana udhaifu. Kwa udhaifu wao, pamoja na udhaifu wa wanaume au wapenzi wenu, wanaweza kuwasaliti. Kwa hiyo ni juu yenu kulinda ndoa zenu, ili udhaifu huo usiwe chanzo kwa kuvunjika kwa matumaini na matarajio yenu ya kujenga familia.Kuna mambo mawili makubwa hapa, kwanza inawezwekana mmejiachia wazi sana kama wanawake na kusahau kuwa wanaume huvutiwa na mambo gani.Kwa hali hiyo, mnawaacha wale walio karibu nao kuwafanyia yale wanayohitaji na kuchukua nafasi zenu.Lakini pili, ni udhaifu wa kibinadamu na zaidi kwa wanaume, linapokuja suala la mwili. Kwa udhaifu huo, inabidi muwasaidie kuwalinda wasishawishiwe kirahisi. Lakini, ndugu zenu wa kike au watumishi mnaoishi nao, inabidi muwakague vizuri na kuacha kuwamini kupita kiasi kwa waume au wapenzi wenu.Ni hatari sana kwa mwanamke kwa mfano, kumwambia au kumruhusu mumewe aende sehemu za starehe na rafiki yake wa kike au na ndugu yake wa kike, ati kwa sababu anamwamini rafiki huyo au mumewe. Kumbuka, suala hapa sio kuaminika au kutoaminika, bali ukweli wa kimaumbile pia. Mwanamke, chunga ndoa yako, ilinde sana, kwani sio dhambi.

Friday, September 2, 2011

NIMEREJEA TENA BAADA YA KIMYA KINGI!

Ni miezi kadhaa na masiku mengi tu sijaonekana katika tasnia hii ya blog. nilipata matatizo ya kifamilia, na nililazimika kusafiri na kukaa Mtwara ukweni kwangu wa muda. nilikuwa kule nikimuuguza mama mke bahati mbaya akafariki lakini sambamba na kifo schake mumewe naye alifariki kwa mshtuko wa kufiwa na mkewe. ulikuwa ni msiba mkubwa sana kwetu.


Sijui ni kuchanganyikiwa au kitu gani nilijikuta nikiwa nimesahau password ya blog yangu, nikakosa mawasiliano kabisa na blog. nilifungua email address nyingine na kuwajulisha kaka Mubelwa na Dada Yasinta nikijaribu kuomba msaada, kwa kweli walijitahidi sana kunisaidia kwa kadiri ya uwezo wao, lakini hawakufanuikiwa.


Ni hivi karibuni nimemudu kupata password yangu nan leo nimerejea tena. sijapata cha kuandika kwa sasa kwa kuwa nilikuwa kwenye mwezi mtukufu, lakini nawaahidi nitarejea muda si mrefu.
Nawapenda na ninawatakia siku njema.


Friday, August 20, 2010

KWA NINI WANAUME WANASHINDWA KULING'AMUA HILI?

Wakikaa kwenye Computer zao, hawana muda na familia

Kuna wakati niliwahi kueleza juu ya wanaume kudhani kuwa kuwanunulia wake au wapenzi wao kila kitu kwa maana ya nyumba nzuri, magari ya kifahari na mavazi ya thamani, inatosha kupeleka ujumbe kwa mke au mpenzi wake kuwa anapendwa.

Nilieleza kwa kirefu sana juu ya dhana hiyo jinsi isivyo sahihi na niliweka bayana kuwa, wanawake ni viumbe wanaohitaji kusikilizwa kuliko kitu kingine, bila shaka mlio wengi mnakumbuka makala hiyo.

Kwa asili wanaume wanapenda sana kuwasikia wake au wapenzi wao wakikiri kuwa wanawapenda na kufurahia tabia zao nzuri wema walio nao, vipaji walivyo navyo na sifa nyingine lukuki.

Wanaume wanapopewa sifa za aina hii na wake au wapenzi wao hufurahia na kupata nguvu na kuona kwamba wana thamani kubwa mbele ya wake au wapenzi wao, kinyume na hivyo wanaume hukerwa na kutowajali wake zao.

Pamoja na kuoneshwa upendo lakini hata hivyo hiyo haitoshi kuwafanya wanaume wawapende na kuwajali wake au wapenzi wao. Kuna wakati mwanaume anakuwa na kazi nyingi sana na anatumia muda mwingi kwenye kujisomea au kuangalia Luninga, hata pale mke au mpenzi wake anaponyesha kwamba anahitaji kuwa naye kwa muda fulani.

Kuna wakati pia mwanaume anajali zaidi kazi zake kuliko mambo mengine ambayo mkewe anayataka na kuyaona ya maana. Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa kauli hizi, “Yaani niache kazi zangu nikae kukusikiliza wewe na upuuzi wako, subiri nikipata muda tutaongea mambo hayo” kauli hizi ni sumu kali sana katika uhusiano, na huchangia kwa kiasi kikubwa ndoa na mahusiano ya wapenzi wengi kuporomoka.

Ni kweli kuwa kuna wakati mwanaume anaweza kuwa bize na shughuli zake,lakini pale mke au mpenzi wake anapohitaji ukaribu na yeye ni wajibu wake kuonesha kujali.Kama mwanamke anahitaji kufanya jambo fulani ambalo inabidi mwanaume amsaidie, lakini inapotokea mwanaume kuonyesha kwamba hajali sana juu ya jambo hilo bila kujali kama yuko bize au hayuko bize, mwanamke huhisi kutothaminiwa na hiyo humuumiza sana kihisia.

Lakini kama mwanaume ataonesha kujali hisia za mkewe na kumsikiliza kwa makini hata kama hatatoa ushirikiano hiyo tu inatosha kumridhisha mke au mpenzi kuhisi kuwa anapendwa na anasikilizwa.Lakini utakuta wanaume wengi hawajali utashi wa kihisia wa wake zao na huamini kwamba wanawake wanachohitaji ni kupewa fedha au mali na kuhakikishiwa maisha ya kifahari basi.

Ukweli ni kwamba wanawake wanahitaji sana kusikilizwa hisia zao na kupewa nafasi pekee na mume au mpenzi wake pale anapohitaji nafasi hiyo ya kusikilizwa. Kumuonesha mwanamke kwamba hana thamani na hana nafasi ya kusikilizwa na badala yake kazi na kusoma, au kuangalia luninga kukaonekana ndio kuna thamani kuliko yeye ni kosa kubwa.

Ni jambo la msingi sana kwa wanaume kulifahamu hili kwa ustawi wa ndoa au mahusiano yao na wake au wapenzi wao, kwani wanawake wanahitaji nafasi kutoka kwa wanaume au wapenzi wao zaidi ya kitu kingine, maana hayo mengine yatakuja kujazia tu.


Makala hii nimeitoa kwa dada yangu Yasinta Ngonyani. Nimeona sio vibaya kuiweka hapa kwangu kwani imenigusa sana. kwa kumsoma dada huyu zaidi waweza kubonyeza HAPA.

Sunday, August 15, 2010

WAZAZI WANAPOGAWANA WATOTO!

Je hawa nao wamegawana watoto?

Je huyu naye ni wa baba?


Yasemekana binti mdogo ndiye kipenzi cha Rais Obama

Kuna dhana imejengeka sana miongoni mwa jamii, na sio hapa nyumbani tu, bali pia hata huko katika nchi za wenzetu, ya wazazi kugawana watoto. Kwa mujibu wa simulizi mbalimbali na kautafiti kangu kadogo nilikofanya, nimegundua kuwa familia nyingi hususan zile zenye watoto wachache wanagawana watoto kimtindo.

Tabia hii inadaiwa kuwepo katika familia yoyote bila kujali rangi, dini wala kabila, ambapo huwa inatokea wazazi wakagawana watoto, yaani kwa mfano inaweza kutokea mzazi wa kiume akawapenda watoto fulani na mzazi wa kike akawapenda watoto fulani.

Kama ikitokea mtoto anayependwa na mama akikosea basi mama atafanya kila namna kumkinga dhidi ya adhabu kutoka kwa baba, na kama ikitokea mtoto ambaye sio kipenzi cha mama akikosea basi baba atapewa mashtaka mara moja, ingawa mara nyingi baba huwa anapuuza au kutoa adhabu ndogo kwa mtoto huyo.

Inadaiwa kwamba hata watoto huijua hali hiyo na hivyo hujua mahali pa kumshitakia mwenzie akikosea, kwa kuamini kwamba atapewa adhabu stahiki.

Inasemekana kwamba kwa familia kubwa yaani yenye watoto wanaozidi wawili ni vigumu hali hiyo kuwa wazi, lakini kwa familia yenye watoto wawili, wazazi hugawana watoto waziwazi, kila mtoto hujidai kwa mzazi ampendae.

Ni jambo la kawaida katika familia yenye watoto wawili, wakike na kiume, kukuta mtoto wa kiume ni kipenzi cha mama na yule wa kike ni kipenzi cha baba. Na kama watoto hao wakiwa ni wa jinsia moja, basi ni lazima kila mzazi atachagua wakwake.

Uchaguzi huo wa watoto usio rasmi huwa unawaweka watoto katika wakati mgumu na kuwasababishia maumivu ya kihisia au kuwaathirika kisaikolojia pale mzazi mmoja anapofariki, kwani yule aliyekuwa akipendwa na mzazi huyo hujiona kama vile hana pa kukimbilia na hivyo kukosa amani.

Je jambo hilo lina ukweli wowote au ni dhana tu iliyopewa nguvu na imani ya kufikirika?

Friday, August 13, 2010

ETI WANAWAKE WAREMBO HUUA?

Hivi inawezekana kweli kwa mrembo kama huyu?

Jana tulikuwa na ubishi hapa kazini kwangu. Ubishi wenyewe ulikuwa unahusiana na wanawake warembo. Kuna mwenzetu mmoja amedai kuwa eti hawezi kuoa mwanamke mzuri sana kwa sababu atakufa mapema. Aliendelea kusema kuwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo, yaani yule anayekubalika kwa viwango vyote na wanaume kuwa ni mzuri, hafai kuolewa bali ni wa kuchezewa tu na wanaume!

Sababu aliyoitoa ni kwamba eti kuoa mwanamke mzuri sana kwa viwango vyote itamletea presha, kwa sababu atakuwa akitamaniwa na kila mwanaume, na mara nyingi kama mume atakua ni mtu wa kipato kidogo, ni rahisi mkewe huyo kuingia katika vishawisi na kutoka nje ya ndoa kwa sababu atakuwa akiwindwa na wanaume wakware.

Alizidi kubainisha kuwa jambo hilo amelifanyia utafiti na kupata ukweli wa kutosha kuwa wanaume wengi waliooa wanawake wazuri kupindukia aidha walifarki kwa maradhi ya moyo wakiwa bado na umri mdogo au wamepata maradhi ya kudumu kama vile presha na kisukari kutokana na hofu ya kuporwa wake zao hao au hata ukimwi.

Hata wale walioachwa na wake zao baada ya kushawaishiwa na wanaume wenye pesa, wengi waliishia kujinyonga au kujiua kwa kunywa sumu, na wengine waliishia kuwa watumiaji wa aidha madawa ya kulevya au matumizi ya pombe kupindukia.

Ukweli ni kwamba kulizuka ubishi mkubwa pale ofisini kati ya wanawake na wanaume kila upande ukitetea upande wake. Nimeona na mie niilete mada hii hapa kibarazani ili kupata maoni ya wasomaji wa kibaraza hiki.

Je jambo hili lina ukweli wowote?

Sunday, August 8, 2010

DALILI ZA WANAWAKE NA WANAUME WANAOSALITI NDOA ZAO HIZI HAPA

Hiki nacho ni kisingizio

Dalili za Mke anayetoka nje ya ndoa:

1) Anatembea na vidonge vya majira kwenye mkoba wake, wakati mume amefanyiwa Vasectomy (Kufunga kizazi kwa mwanaume)
2) Anakuwa na namba ya siri ya simu ambayo mume haijui
3) Anatumia muda mwingi anapokwenda sokoni au kufanya manunuzi ya wiki
4) Anajinunulia nguo za gharama zikiwemo nguo za ndani bila kumshirikisha mume
5) Anakuwa akitegemea zaidi ushauri kutoka nje kwa watu wengine zaidi ya mumewe
6) Anaacha kuvaa pete ya ndoa bila sababu
7) Anapopigiwa simu akiwa karibu na mumewe anaizima au kwenda kupokelea nje
8) Anakuwa hajali tena mambo ya familia na hujiamulia mambo yake mwenyewe
9) Ni rahisi sana kusema ‘nipe talaka yangu’ inapotokea kutofautiana hata kwa jambo dogo.
10) Dharau na kejeli kwa mume hujionyesha waziwazi


Dalili za mume anayetoka nje ya ndoa:

1) Unakuta Condom kwenye mkoba wake au kwenye gari lake wakati umefunga kizazi au unatumia vidonge vya majira.
2) Anapunguza au anaacha kabisa kuwa outing na familia yake
3) Unakuta lipstick kwenye kiti cha gari lake ambayo huifahamu
4) Ghafla anataka mjaribu aina mpya ya kufanya mapenzi
5) Anafanya kazi masaa mengi ya ziada lakini malipo hayaonekani kwenye salary slip
6) Hali au anakula kidogo sana nyumbani kwa kuwa ameshakula kwa nyumba ndogo
7) Nguo zake zinanukia manukato (Perfume)ambayo hata huyafahamu
8) Unakuta alama ya lipstick kwenye shati lake
9) Anakuwa na namba ya siri ya simu na wakati mwingine zaidi ya tatu ambazo mke hazijui
10) Anapopigiwa simu akiwa karibu na mkewe anaizima au kwenda kupokelea nje

Sunday, August 1, 2010

LIKIZO YANGU MIKOA YA KUSINI NA UTAFITI WANGU UCHWARA!

Daraja la Mkapa


Barabara ilikuwa haipitiki

Viunga vya Mtwara

Kimya changu nilikuwa likizo huko mikoa ya kusini. Ilikuwa ni likizo ndefu kidogo ambapo nilipata fursa ya kuwatembelea wakwe zangu niliopoteana nao kwa miaka kadhaa iliyopita.

Pamoja na likizo lakini nilitumia muda wangu kujifunza mambo mengi ambayo kama nitapata fursa, basi nitawashirikisha ili tujadili kwa pamoja.

Hali ya barabara si ya kuridhisha ingawa wenyeji waliniambia kuwa hali kwa sasa ni ya afadhali ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Kwa mfano kutoka Ikwiriri lilipo daraja la Mkapa mpaka Somanga ni kama Kilomita 60, na kipande hicho hakina lami, wakati tunakwenda huko kulikua na hali ya mvua hivyo barabara ilikuwa inateleza sana.

Hata hivyo nilivutiwa sana na Daraja la Mkapa ambalo kwa kweli ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuliona tangu lilipojengwa. Kutokana na kuliona daraja hilo, nikajikuta nikihesabu idadi ya madaraja nikianzia Mtwara.

Inawezekana nisiwe sahihi sana lakini kulingana na hesabu zangu nimepata idadi ya madaraja ifuatayo:

Kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja nilipata idadi ya madaraja 5
Kutoka Mnazi Mmoja hadi Lindi nilipata idadi ya madaraja 6
Kutoka Lindi hadi Kibiti nilipata idadi ya madaraja 79

Pamoja na idadi hiyo ya madaraja, pia yapo yanayojengwa, ambayo ni yale ya kutoka Somanga hadi Daraja la mkapa nilipata idadi ya madaraja 45.
Kutoka Daraja la Mkapa hadi Dar nilipata idadi ya madaraja 17

Ukijumlisha hiyo idadi ya madaraja unapata jumla ya madaraja 152. kwa umbali wa kilomita 554, yaani kutoka Dar hadi Mtwara!

Naambiwa kuwa gharama za ujenzi wa barabara huwa zinakuwa kubwa kulingana na idadi ya madaraja yatakayojengwa. Hapo ndipo nilipowaza kuwa isije kuwa kuchelewa kujengwa kwa barabara za mikoa ya kusini kulichangiwa zaidi na idadi ya madaraja kuwa mengi, ukilinganisha na mikoa mingine hususan ya kaskazini.

Kwa mujibu mdogo wangu Koero ameniambia kuwa kutoka Dar hadi Arusha ni kilomita 659, alinifafanulia kuwa kutoka Dar hadi Moshi ni kilomita 570, na kutoka Moshi hadi Arusha ni kilomita 89, ukijumlisha unapata hizo kilomita 659, ambapo alikanusha pia kuwa hakuna idadi nyingi ya madaraja ukilinganisha na huko mikoa ya kusini.

Ni kautafiti kadogo ambako nimekafanya wakati wa likizo yangu na ndio sababu ya kuweka hapa kibarazani ili mwenye kufahamu zaidi aweke changamoto yake hapa.

Nikipata muda nitawasimulia vijimambo nilivyokutana navyo huko ukweni, si mnanijua siishi visa!