Sunday, August 15, 2010

WAZAZI WANAPOGAWANA WATOTO!

Je hawa nao wamegawana watoto?

Je huyu naye ni wa baba?


Yasemekana binti mdogo ndiye kipenzi cha Rais Obama

Kuna dhana imejengeka sana miongoni mwa jamii, na sio hapa nyumbani tu, bali pia hata huko katika nchi za wenzetu, ya wazazi kugawana watoto. Kwa mujibu wa simulizi mbalimbali na kautafiti kangu kadogo nilikofanya, nimegundua kuwa familia nyingi hususan zile zenye watoto wachache wanagawana watoto kimtindo.

Tabia hii inadaiwa kuwepo katika familia yoyote bila kujali rangi, dini wala kabila, ambapo huwa inatokea wazazi wakagawana watoto, yaani kwa mfano inaweza kutokea mzazi wa kiume akawapenda watoto fulani na mzazi wa kike akawapenda watoto fulani.

Kama ikitokea mtoto anayependwa na mama akikosea basi mama atafanya kila namna kumkinga dhidi ya adhabu kutoka kwa baba, na kama ikitokea mtoto ambaye sio kipenzi cha mama akikosea basi baba atapewa mashtaka mara moja, ingawa mara nyingi baba huwa anapuuza au kutoa adhabu ndogo kwa mtoto huyo.

Inadaiwa kwamba hata watoto huijua hali hiyo na hivyo hujua mahali pa kumshitakia mwenzie akikosea, kwa kuamini kwamba atapewa adhabu stahiki.

Inasemekana kwamba kwa familia kubwa yaani yenye watoto wanaozidi wawili ni vigumu hali hiyo kuwa wazi, lakini kwa familia yenye watoto wawili, wazazi hugawana watoto waziwazi, kila mtoto hujidai kwa mzazi ampendae.

Ni jambo la kawaida katika familia yenye watoto wawili, wakike na kiume, kukuta mtoto wa kiume ni kipenzi cha mama na yule wa kike ni kipenzi cha baba. Na kama watoto hao wakiwa ni wa jinsia moja, basi ni lazima kila mzazi atachagua wakwake.

Uchaguzi huo wa watoto usio rasmi huwa unawaweka watoto katika wakati mgumu na kuwasababishia maumivu ya kihisia au kuwaathirika kisaikolojia pale mzazi mmoja anapofariki, kwani yule aliyekuwa akipendwa na mzazi huyo hujiona kama vile hana pa kukimbilia na hivyo kukosa amani.

Je jambo hilo lina ukweli wowote au ni dhana tu iliyopewa nguvu na imani ya kufikirika?

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ha ha ha ! kaazi kwelikweli. Hii kali nimewahi kusikia na wala siiamini kwani binafsi mtoto ni mtoto na nawapenda wote sawasawa kabisa. Na nadhani ni imani tu ya watu. Ni mtizamo wangu na ni ruksa kibisha

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Inategemea na mrengo wako...kama ni wa kushoto haya kama ni wa kulia haya...lol!

Kumbuka kila mrengo una athari zake..lol!

Koero Mkundi said...

sie kwetu tuko wengi kidogo, lakini sie wa mwisho, yaani mie na mdogo wangu wa kiume niliyemtangulia, wazazi wametugawana, mie nimegundua kuwa baba ananipendelea na mdogo wangu wa mwisho wa kiume anapendelewa na mama.
kwa hiyo hilo jambo mie naona lina ukweli kidogo....

emu-three said...

Unajua kama mzazi huwezi kugawa watoto, kwa uzoefu wangu kama mzazi, hilo kama lipo basi ni wazazi ambao umakini wa athari kwa mtoto hawaujali.
Kinachotokea ni kuwa baadhi ya watoto wanapenda kutendewa jambo fulani, huenda mama anamkubalia kila akitaka hilo tendo, lakini akienda kwa baba anamkatalia kwasababu baba anajua athari zake au ameonelea kuwa halifai. Kwa mtizamo wa kitoto lazima ataona kuna upendeleo fulani, na ichukuliwe kuwa baba alimkatalia yeye na akampa mwingine.
Kwa nini baba alimpa mwingine kwasababu kuna kuangalia huyu anafaa hiki au hafai kile, huyu ana mawazao mapana huyu bado hajakomaa, kama mzazi lazima uwe na busara hiyo.
Kuna wengine hudai baba mara nyingi anapendelea watoto wa kike na mama watoto wa kiume hiyo ni nadharia tu ya kitoto, yaani sisi tukipeleka malalamiko kwa mama anatusikiliza, ndio kwa mama itakuwa wepesi kuwasikiliza watotoo wa kiume kwasababu hujuzi wake kwa watoto wa kiume unaishia kwenye `utoto' lakini unadani na ukubwa wa mambo ya kiume anayejua zaidi ni baba, kwasababau yeye ni mwanaume.
Halikadhalika kwa watoto wa kike wakienda kwa baba atawakubalia kirahisi lakini kwa mama atafikiria mara mbili, anajua akiwadekeza kwa hili au lile wataharibika lazima awe mkali kwasababu ya uzoefu wa `uuke'
Nafikiri nimejaribu kuelezea kiuzoefu wangu tu, kwasababu nami nina watoto wakike na kiume

Mija Shija Sayi said...

Safi sana emu-three.