Thursday, May 27, 2010

INAKUWAJE TUNAIVAA MIKENGE?

Tunavumilia mengi kwa kweli

Nimefarijika sana kwa mapokezi makubwa niliyoyapata katika tasnia hii ya blog. Ni jambo la kujivunia kupata ukarimu kwa watu hata usiofahamiana nao. Nawashukuru sana.

Leo nimekuja na jambo lingine ambalo nimekuwa nikijiuliza siku nyingi, lakini sijapata majibu ya kuridhisha. Pamoja na kuwashirikisha baadhi ya mashoga zangu lakini wameshindwa kunipa majibu muafaka.

Jambo lenyewe linahusiana na sisi wanawake, na ningependa wanaume nao watoe mtazamo wao juu ya jambo hili.

Linapokuja swala la kuchagua mchumba, kwa kawaida wanawake huwa tunakuwa makini sana. Kwani kila mwanamke na hata wanaume wanakuwa na matarajio yao linapokuja swala la kuchagua mwenza.

Pale anapotokea mwanamke kuposwa, lakini naomba hapa mnielewe, sizungumzii ule mtindo wa kuonjwa ndipo mtu aamue kuchonga mzinga. La hasha, nazungumzia swala zima la mchakato wa kufahamiana na msichana hadi kufikia hatua ya kuchumbia hadi kuoana.

Kama nilivyosema awali kuwa katika mchakato wa kuchagua mchumba sisi wanawake tunakuwa ni waangalifu kweli na lengo kuu ni kutaka ndoto zetu zitimie, si kila mtu anazo ndoto zake? Kuna wanaotaka wanaume wazuri kwa sura, na wajasiri, wasiopenda makuu au wachangamfu na wenye bashasha, wasio wabahili….Maana kuna wanaume wabahaili ajabu lakini pamoja na ubahili wao hawana malengo….dada Yasinta anasemaga Kaaazi kweli kweli.

Lakini mara nyingi utakuta wanawakwe wengi wanajikuta wanaivaa mikenge na kuolewa na wanaume ambao sio matarajio yao.

Nimejaribu kuongea na wanawake wenzangu ambao wako kwenye ndoa, wengi wamekiri kuwa waume zao kabla ya kuoana walikuwa na sifa zote walizozitaka, na waliamini kuwa wamefika Kigoma mwisho wa reli, lakini baada ya kuoana ndio segere likaanza.

Wanawake wengi wanadai kuwa, baadhi ya wanaume wanapotaka kuoa huwa kama kinyonga, yaani hubadilika kulingana na jinsi anavyomsoma mwanamke aliyevutiwa naye.

Kwa mfano kama mwanamke anayemtamani kuwa na uhusiano naye anapenda mwanaume mwenye sifa fulani, basi atajitahidi kubeba ile sifa ya bandia mpaka ampate mwanamke huyo, lakini baada ya kuoana ndipo mambo hugeuka, kwani zile sifa zote chafu na zenye kukera zitaanza kudhihiri.

Yupo shoga yangu mmoja aliwahi kunichekesha kuwa mumewe alijifanya mlokole na walipooana ulokole ulitoweka baada ya miezi sita, yaani mumewe alirudia tabia zake za ulevi, uzinzi, na tabia nyingine mbaya tofauti na ulokole.

Kwa sisi waislamu ni rahisi mtu kujiondoa kwenye ndoa ambayo huridhiki nayo, kwani hatufungwi sana na ndoa kama wenzetu wakristo ambao huapa kanisani kwa kusema, ‘mpaka kifo kitakapotutenganisha’

Kwetu sisi waislamu, ingawa sio wengi wanaoweza kuwa na ujasiri huo, kujitoa kwenye ndoa ngumu au iliyo kinyume na matarajio yako ni rahisi zaidi ukilinganisha na wenzetu wakristo, kwani ni rahisi sana kubwaga manyanga na kujiondokea.

Lakini pia swala hilo lisichukuliwe kuwa ni rahisi sana ki hivyo, bali kuna kamchakato ambako inabidi kafanyike hadi ndoa kuvunjika na kila mtu kuishi kivyake.

Ninachotaka kujua hapa ni, je kwa nini kunakuwa na unafiki sana kwa wanaume linapokuja swala la kuchumbia?