Sunday, June 20, 2010

UCHAWI NILIOWAHI KUUSHUHUDIA!

Mara nyingi hawa ndio walengwa


Niliushuhudia hapa!

Kuna simulizi nyingi sana kuhusiana na mila zetu za Kiafrika na vijimambo vyake, hususana mambo ya kishirikina au uchawi. Kama utataka kuandika mada ya Uchawi au ushirikina hasa kwa sisi Waafrika, basi utajaza vitabu lukuki.

Katika kukua kwangu, nimekutana na mambo mengi sana na simulizi nyingi zinazohusiana na ushirikina au uchawi. Zipo niliyowahi kusimuliwa na nyingine nimewahi kushuhudia mwenyewe kwa macho yangu.

Nisingependa kuzungumzia yale niliyowahi kuyashuhudia mwenyewe kwa undani kwa sababu yanaweza kuwagusa baadhi ya watu ambao kama wakisoma habari hii hawatajisikia vizuri na nisingependa kuwakera watu na kuwa sehemu ya tatizo.
Leo hii ningependa kuzungumzia baadhi ya mambo ya kishirikina au uchawi kwa kuangalia baadhi ya mikoa ambayo nimewahi kuishi na kushuhudia au kusimuliwa.

Kwa Kule Tanga, kuna uchawi ambao huitwa Zongo ambapo walengwa wakubwa ni watoto wadogo wanaonzia uchanga hadi miaka kama sikosei kumi. Ingawa aina hii ya uchawi inahusishwa na macho mabaya yaani inavyosemekana ni kwamba kuna watu ambao wana macho yenye kudhuru kama ilivyo kwenye kauli. Kuna w2atu ambao wakitamka neno ni lazima litaokea na watu hawa wamekuwa wakihusishwa na uchawi wakati sio kweli, ingawa pia wapo watu ambao huwa ni wachawi kweli.

Nikirudi kwenye swala la macho mabaya yenye kudhuru, ni kwamba watu hawa inasemekana wanauwezo hata wa kusababisha mimba changa kutoka bila wao kukusudia, lakini kwa Mkoani Tanga huo ni uchawi kabisa ambao watu huununua na kuutumia kuwadhuru wengine, hususana watoto.

Inasemekana kuwa watu wenye kutumia uchawi huo wa zongo huwatupia watoto ambapo mtoto anayetupiwa uchawi huo anaweza kuandamwa na homa kali na hata kutopata choo na tumbo kuuma sana.

Mtoto anayetupiwa uchawi huo hawezi kutibiwa kwa dawa za hospitali, na majaaliwa ya kupona kwake ni kupelekwa kwa mtaalamu wa mitishamba wa kutibu zongo. Lakini pia kwa wale wazee wa zamani wanajua tiba hiyo ambapo haihitaji sana kupelekwe kwa mtaalamu.

Kwa kutumia Tula au wengine huita Ndulele na ufagio ule wa kizamani na sio hii ya Shoprite au Mlimani City, unaweza kutibu hilo zongo. Simulizi hii niliwahi kusimuliwa na shoga yangu mwenyeji wa huko Handeni, na kama maelezo yangu hayako sahihi basi wenyeji wa mkoa huo wanaofahamu zaidi watanisahihisha.

Na kwa kule Moshi, nadhani na Arusha watu hao wenye macho mabaya huwa wanajijua na hata jamii inayowazunguka huwa inawajua. Nilisimuliwa kwamba, kwa mfano kama mtu mwnye macho hayo mabaya anakwenda kumtembelea mama aliyejifungua, kwa kule Moshi, mama mwenye macho mabaya hupewa kwanza kipande cha mgomba akipakate, mfano wa kama amepakata mtoto, kisha ndipo apewe mtoto halisi ampakate. Lengo ni kuhakikisha kuwa mtoto hadhuriwi na macho ya mtu huyo.

Wakati mwingine watu hao wenye macho mabaya hukiri kabisa kuwa wana macho mabaya ili watu waliomzunguka wafahamu hivyo, kuepusha lawama. Naomba dada Subi ayaweke sawa maelezo yangu kama nitakuwa nimekosea.

Kule Pangani napo pamoja na uchawi wa zongo ambao nadhani karibu Mkoa wa Tanga wote unafanyika, pia niliwahi kukutana na uchawi maarufu kama Kopea.
Uchawi huu ukoje? Inasemekana watu wanaotumia uchawi huu ni vijana na wazee na uchawi wenyewe unahusiana na chakula.

Inakuwaje? Ni hivi, kwa mfano unaweza kwenda kwenye mghahawa na kuagiza chakula, basi anaweza akatokea mtu akaja na kukaa jirani na wewe akawa anakuangalia unavyokula kwa jicho la wizi. Utakapomaliza na kulipa ukishatoka nje ya mghahawa huo unajisikia njaa kama vile hujala kitu.

Hiyo ina maana kwamba, umekula wewe lakini aliyeshiba ni mwingine, yaani yule mtu aliyekaa jirani na wewe wakati unakula ambaye aliyekuwa anakuangalia kwa jicho la wizi.

Kwa Pangani huo uchawi unachukuliwa kama mchezo tu ambao wenyeji huufanya kwa mazoea, ingawa haudhuru. Kwa wale wenye mighahawa mjini Pangani wanawajua watu wenye tabia hizo na mara nyingi wakiwaona huwatoa nje kwa sababu ya kuepuka kupotezewa wateja.

Mpaka hapo nadhani utakuwa umepata picha juu ya swala zima la ushirikina na vijimambo vyake.