Sunday, August 15, 2010

WAZAZI WANAPOGAWANA WATOTO!

Je hawa nao wamegawana watoto?

Je huyu naye ni wa baba?


Yasemekana binti mdogo ndiye kipenzi cha Rais Obama

Kuna dhana imejengeka sana miongoni mwa jamii, na sio hapa nyumbani tu, bali pia hata huko katika nchi za wenzetu, ya wazazi kugawana watoto. Kwa mujibu wa simulizi mbalimbali na kautafiti kangu kadogo nilikofanya, nimegundua kuwa familia nyingi hususan zile zenye watoto wachache wanagawana watoto kimtindo.

Tabia hii inadaiwa kuwepo katika familia yoyote bila kujali rangi, dini wala kabila, ambapo huwa inatokea wazazi wakagawana watoto, yaani kwa mfano inaweza kutokea mzazi wa kiume akawapenda watoto fulani na mzazi wa kike akawapenda watoto fulani.

Kama ikitokea mtoto anayependwa na mama akikosea basi mama atafanya kila namna kumkinga dhidi ya adhabu kutoka kwa baba, na kama ikitokea mtoto ambaye sio kipenzi cha mama akikosea basi baba atapewa mashtaka mara moja, ingawa mara nyingi baba huwa anapuuza au kutoa adhabu ndogo kwa mtoto huyo.

Inadaiwa kwamba hata watoto huijua hali hiyo na hivyo hujua mahali pa kumshitakia mwenzie akikosea, kwa kuamini kwamba atapewa adhabu stahiki.

Inasemekana kwamba kwa familia kubwa yaani yenye watoto wanaozidi wawili ni vigumu hali hiyo kuwa wazi, lakini kwa familia yenye watoto wawili, wazazi hugawana watoto waziwazi, kila mtoto hujidai kwa mzazi ampendae.

Ni jambo la kawaida katika familia yenye watoto wawili, wakike na kiume, kukuta mtoto wa kiume ni kipenzi cha mama na yule wa kike ni kipenzi cha baba. Na kama watoto hao wakiwa ni wa jinsia moja, basi ni lazima kila mzazi atachagua wakwake.

Uchaguzi huo wa watoto usio rasmi huwa unawaweka watoto katika wakati mgumu na kuwasababishia maumivu ya kihisia au kuwaathirika kisaikolojia pale mzazi mmoja anapofariki, kwani yule aliyekuwa akipendwa na mzazi huyo hujiona kama vile hana pa kukimbilia na hivyo kukosa amani.

Je jambo hilo lina ukweli wowote au ni dhana tu iliyopewa nguvu na imani ya kufikirika?