Sunday, June 6, 2010

NI KUBEMENDWA AU NI UTAPIAMLO?

Eti Kamebemendwa!

Kwanza naomba radhi kwa kutoonekana kwangu mtandaoni bila taarifa, ni jambo la kusikitisha kwamba, kungali bado mapema lakini nimeanza kutoonekana mtandaoni na hivyo kuwafanya wadau wenzangu na wasomaji wajiulize kulikoni.

Kutoonekana kwangu mtandaoni, ni kutokana na kuhudhuiria shughuli ya mdogo wangu kuchezwa unyago na hivyo kulazimika kuhudhuria mwanzo mwisho. Si mnajua mambo ya mila! Lakini hili nitalizungumzia wakati mwingine, kwa sasa ngoja nizungumzie jambo lingine ambalo nalo linafikirisha.

Kuna visa asili vingi ambavyo huwa wakati mwingine vinaniacha na maswali lukuki. Jambo ninalotaka kulizungumzia leo, limekuwa likiaminiwa sana na jamii yetu na limekuwa likionekana kama vile ni jambo la kweli kabisa.

Ni hivi karibuni nimejikuta nikianza kulitilia mashaka, na nimeona leo niwashirikishe wadau na wasomaji wenzangu katika kutafakari juu ya jambo hili ili kujua kama kweli lina ukweli wowote au ni mambo tu yaliyopewa nguvu na jamii kiasi cha kuaminiwa kuwa na ukweli wakati huenda halina ukweli wowote.

Swala la mwanamke wa Kiafrika kubeba mimba huwa linaambatana na mambo mengi ya kimila ambayo yametengenezwa na jamii ili kuhakikisha kwamba kiumbe aliyeko tumboni mwa manamke anakuwa salama salimini kuanzia tangu kutunga mimba mpaka kuzaliwa. Na si hivyo tu, hata pale mtoto anapozaliwa bado kuna taratibu nyiingi sana za mila na desturi zitafuata ili mtoto huyo akue akiwa salama.

Naamini hakuna aisyejua juu ya taratibu nyingi ambazo karibu kila kabila hapa nchini huzifuata linapokuja swala la uzazi na malezi ya watoto wetu. Labda nikiri kuwa mie binafsi nimekuwa nikifuata baadhi ya mila hizi karibu kwa watoto wangu wote watatu tangu kutungwa kwa mimba hadi kuzaliwa na hata katika malezi kwa ujumla.

Ni hivi karibuni, nadhani ni baada ya kujielimisha kidogo kupitia kwa watu mbalimbali wenye mila na desturi tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na mtandao, ndipo nikajikuta nikianza kuzitilia mashaka baadhi ya mila zetu hizi.

Jambo ambalo ningependa kulizungmzia leo ni hili linaloitwa Kubemenda mtoto, sijui kama kuna neno lingine ambao linatumika katika kulielezea jambo hilo lakini mimi ninafahamu zaidi hili neno la Kubemenda.

Inasemwa kuwa Kubemenda mtoto ni kitendo cha mama au baba wa mtoto kutoka nje ya ndoa na kisha kumpakata au kumnyonyesha mtoto bila kuoga lile jasho alilotoka nalo huko alikotoka, kwa sisi waislamu tunaita Janaba.

Inasemwa kuwa Jasho hilo lnasababisha mtoto kudhoofika sana na kupelekea kuchelewa kukua kulingana na umri wake. Watoto wanaotajwa kuwa Wamebemendwa unaweza kuwafananisha na wale wenye tatizo la Utapiamlo yaani Kwashiorkor.

Kwa huku kwetu uswahilini wanaitwa mafundi viatu, kwa maana ya kwamba, unaweza kumuweka mtoto huyo hapo na ukamkuta hapo hapo, kwani hawana uwezo wa kujongea hata kidogo kutokana na kudhoofika sana.

Mara nyingi hasa kwa kule vijijini utakuta watoto wanafungwa dawa mikononi na viunoni ili kuepushwa na mambo mabaya ya kishirikina ikiwepo kukingwa na Kubemendwa iwapo mmoja kati ya wanandoa ametoka nje na akajisahau na kumshika au kumapakata mtoto. Inasemwa pia kuwa hata mtu baki ambaye analo jasho hilo la Janaba linaweza kumdhuru mtoto, iwapo atampakata.

Ninavyofahamu mimi mtoto anaweza kudhoofika na kuchewa kukua kutokana na ugonjwa wa utapiamlo (Kwashiorkor) ambao unatokana na lishe duni, yaani kutopewa vyakula vyenye viini lishe. Swala la Kubemendwa nadhani linaweza kuhusishwa na mwanamke aliyejifungua kubeba mimba wakati mtoto akiwa bado mdogo na ananyonya, kwani maziwa ya mama mjamzito yanadaiwa kuwa yanaweza kumdhuru mtoto.

Kutokana na jambo hilo kusemwa sana na kupewa uzito katika jamii yetu nimeona leo niliweke hapa barazani ili kwa pamoja tulijadili na kuliweka bayana kama litakuwa na ukweli wowote au kuna sababu nyingine.

Karibuni tujadili kwa pamoja.