Friday, August 13, 2010

ETI WANAWAKE WAREMBO HUUA?

Hivi inawezekana kweli kwa mrembo kama huyu?

Jana tulikuwa na ubishi hapa kazini kwangu. Ubishi wenyewe ulikuwa unahusiana na wanawake warembo. Kuna mwenzetu mmoja amedai kuwa eti hawezi kuoa mwanamke mzuri sana kwa sababu atakufa mapema. Aliendelea kusema kuwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo, yaani yule anayekubalika kwa viwango vyote na wanaume kuwa ni mzuri, hafai kuolewa bali ni wa kuchezewa tu na wanaume!

Sababu aliyoitoa ni kwamba eti kuoa mwanamke mzuri sana kwa viwango vyote itamletea presha, kwa sababu atakuwa akitamaniwa na kila mwanaume, na mara nyingi kama mume atakua ni mtu wa kipato kidogo, ni rahisi mkewe huyo kuingia katika vishawisi na kutoka nje ya ndoa kwa sababu atakuwa akiwindwa na wanaume wakware.

Alizidi kubainisha kuwa jambo hilo amelifanyia utafiti na kupata ukweli wa kutosha kuwa wanaume wengi waliooa wanawake wazuri kupindukia aidha walifarki kwa maradhi ya moyo wakiwa bado na umri mdogo au wamepata maradhi ya kudumu kama vile presha na kisukari kutokana na hofu ya kuporwa wake zao hao au hata ukimwi.

Hata wale walioachwa na wake zao baada ya kushawaishiwa na wanaume wenye pesa, wengi waliishia kujinyonga au kujiua kwa kunywa sumu, na wengine waliishia kuwa watumiaji wa aidha madawa ya kulevya au matumizi ya pombe kupindukia.

Ukweli ni kwamba kulizuka ubishi mkubwa pale ofisini kati ya wanawake na wanaume kila upande ukitetea upande wake. Nimeona na mie niilete mada hii hapa kibarazani ili kupata maoni ya wasomaji wa kibaraza hiki.

Je jambo hili lina ukweli wowote?